Visit Website

Kwa mahitaji ya mitihani, Maazimio ya kazi, Shajara, Notes, na materials mbalimbali ya kielimu, wasiliana nasi ujipatie huduma zetu kwa gharama nafuu sana.

Tunatoa huduma za materials mbalimbali za kielimu kwa gharama nafuu wasiliana nasi leo..

[PDF] Nukuu za somo sayansi darasa la tatu

nukuu za somo sayansi darasa la 3 | download nukuu za syansi darasa la tatu pdf | nukuu za somo la sayansi darasa la tatu pdf download notes

nukuu za somo sayansi darasa la tatu pdf downoad | nukuu za somo sayansi pdf | sayansi darasa la tatu pdf download


Sura ya Kwanza: Dhana ya sayansi

Maana ya sayansi

Sayansi ni maarifa yanayopatikana kwa kufanya uchunguzi na majaribio. Majaribio yanaweza kuhusisha upimaji wa vitu mbalimbali kama vile jotoridi, urefu na uzito. Sayansi inahusu uchunguzi juu ya mambo mbalimbali. Sayansi hutumika kuelezea jinsi matukio mengi katika mazingira yanavyofanyika. Mifano ya matukio hayo ni kama vile mvua kunyesha, tetemeko la ardhi na kutokea kwa radi. Aidha, sayansi husaidia kutengeneza vifaa vinavyotumika kurahisisha kazi katika maisha ya kila siku. Pia, kutatua matatizo kwa kuzingatia kanuni maalumu.

Matawi ya sayansi

Sayansi ina matawi mbalimbali ambapo kila tawi linahusika na aina fulani ya maarifa. Matawi hayo ya sayansi yanajumuisha Baiolojia, Fizikia na Kemia.

Matawi ya sayansi

Baiolojia

ni tawi la sayansi linalohusu viumbehai. Viumbehai hujumuisha mimea na wanyama.

 

Fizikia

ni tawi la sayansi linalohusu uhusiano wa maada na nishati. Aina za nishati ni pamoja na joto, mwanga na umeme. Kuna vyanzo mbalimbali vya nishati. Jua ndio chanzo kikuu cha nishati.

 

Kemia

ni tawi la sayansi linalohusu muundo na tabia za maada. Pia, inahusisha mabadiliko yanayotokea katika maada. Kuna hali mbalimbali za maada ikiwemo yabisi, kimiminika na gesi. Mfano wa yabisi ni jiwe na sukari. Vimiminika ni kama vile maji na sharubati. Mfano wa gesi ni hewa na gesi ya oksijeni.

 

 

Kielelezo: hali za maada




Umuhimu wa sayansi

Sayansi ni muhimu katika maisha ya kila siku. Ugunduzi wa kisayansi umemwezesha binadamu kumudu mazingira ya nchi kavu, majini na angani. Umuhimu wa sayansi katika maisha ya kila siku ni kama ifuatavyo:

a)   Sayansi husaidia kujenga maarifa na stadi mbalimbali. Mfano wa stadi hizo ni kama vile ubunifu, udadisi na fikra yakinifu.

b)      Kutengeneza vifaa na vitu vinavyotumika katika maisha ya kila siku kwa mfano:

        i.            Kutengeneza vitu na vifaa vinavyotumika nyumbani kama vile nguo, sabuni, dawa za kusafishia meno, jiko la gesi, mitungi ya gesi, meza, vyombo vya chakula, televisheni, jokofu na redio

      ii.           Kutengeneza vitu vinavyotumika shuleni kama vile chaki, daftari, kalamu na vitabu.

    iii.            Kutengeneza vifaa vya ujenzi kama vile saruji, chokaa, mabati, mabomba, chuma na marumaru vinavyotumika katika ujenzi wa nyumba

Kutengeneza vifaa vya kufanyia uchunguzi na utambuzi wa magonjwa na tiba

Kutengeneza vifaa vya kurahisisha mawasiliano. Kwa mfano simu na kompyuta vinavyotumika kuwasiliana

 

Taaluma zinazohusiana na sayansi

Zipo taaluma mbalimbali zinazotokana na kujifunza sayansi. Taaluma hizo ni kama vile ualimu, ufamasia, uhandisi, udaktari wa wanyama, udaktari wa binadamu, urubani, ukemia na utaalamu wa mimea.

Jedwali: Taaluma zinazohusiana na sayansi

Na.

Taaluma

Maelezo ya taaluma

1

Udaktari wa binadamu

Taaluma inayohusu kutibu binadamu. Mtaalamu huitwa daktari wa binadamu.

2

Ualimu

Taaluma inayohusu kufundisha sayansi. Mtaalamu huitwa mwalimu.

3

Ufamasia

Taaluma inayohusu kutengeneza, kutoa na kusimamia matumizi ya dawa. Mtaalamu huitwa mfamasia.

4

Uhandisi

Taaluma inayohusu ubunifu wa kutengeneza miundombinu. Mtaalamu huitwa mhandisi.

5

Utaalamu wa kemia

Taaluma inayohusu utengenezaji na uchunguzi wa kemikali. Mtaalamu huitwa mkemia.

6

Utaalamu wa mimea

Taaluma inayohusu sayansi ya mimea. Mtaalamu huitwa mtaalamu wa mimea.

7

Udaktari wa wanyama

Taaluma inayohusu tiba kwa wanyama. Mtaalamu huitwa daktari wa wanyama.





Sura ya Pili: Milango ya fahamu

Maana ya milango ya fahamu Mazingira yetu yana vitu vyenye vichocheo mbalimbali. Milango ya fahamu inasaidia kutambua vichocheo hivyo. Kwa binadamu, milango ya fahamu ni ogani zenye uwezo wa kupokea vichocheo na kupeleka taarifa katika mfumo wa fahamu. Taarifa za vichocheo hutafsiriwa kwenye ubongo. Kielelezo namba 1 kinaonesha milango ya fahamu ambayo ni jicho, sikio, ngozi, pua na ulimi.



Kielelezo:milango ya fahamu

kazi za milango ya fahamu

Macho

Macho hutumika kuona na kutambua vitu. Macho yapo sehemu ya mbele ya uso. Macho hushikiliwa katika sehemu yake kwa misuli. Misuli hii hulifanya jicho liwe na uwezo wa kutazama pande mbalimbali.

Sehemu za jicho

Jicho la binadamu limeundwa na sehemu kuu mbili. Sehemu hizo ni sehemu ya nje na sehemu ya ndani. Sehemu ya nje imeundwa na nyusi, vifuniko vya jicho na kope.

 


Kielelezo:sehemu ya nje ya jicho

Sehemu ya ndani inajumuisha mboni au irisi, pupili, lenzi na retina. Pupili huruhusu mwanga kuingia ndani ya jicho. Mboni hurekebisha kiwango cha mwanga kinachoingia kwenye jicho kwa kutanuka na kusinyaa. Retina hupokea mwanga. Taarifa hiyo ya mwanga husafirishwa mpaka kwenye ubongo ili itafsiriwe na kuwa taswira tunayoiona.

 


Kielelezo:sehemu ya ndani ya jicho


Sehemu za jicho na kazi zake

Sehemu za jicho zina kazi mbalimbali zinazowezesha jicho kuona vema

Jedwali:sehemu za jicho na kazi zake

Sehemu kuu ya jicho

Sehemu kuu ya jicho

kazi

Sehemu ya nje

Nyusi

Huzuia jasho, vumbi na vitu vingine kuingia ndani ya jicho.

Vifuniko vya jicho

Vinafunika jicho ili kuzuia vitu kuingia ndani yake.

Kope

Zinazuia vumbi kuingia ndani ya jicho.

Sehemu ya ndani

Pupili

Huruhusu mwanga kuingia kwenye jicho.

Mboni

Hurekebisha kiwango cha mwanga kinachoingia kwenye jicho.

Retina

Hupokea mwanga. Mwanga huo huwezesha kufanyika kwa taswira.

Lenzi

Kupitisha mwanga na kuupindisha ili utue kwenye retina na kuwezesha taswira ya kitu kufanyika.

 

Utunzaji wa macho

Utunzaji wa macho ni muhimu ili kuendelea kuona vizuri. Mambo ya kuzingatia kuhusu utunzaji wa macho ni:

a)      Usivae miwani bila ushauri wa daktari.

b)      Unaposoma kaa kwenye mwanga wa kutosha

c)      Safisha macho mara kwa mara kwa maji safi

d)      Usifute macho kwa mikono au kitambaa kichafu

 

Ulimi Ulimi

ni ogani inayohusika na kutambua ladha za vitu mbalimbali. Uwezo huu hutokana na kuwepo kwa seli onji zilizo katika ulimi. Ulimi hutambua ladha tano ambazo ni ladha ya utamu, uchachu, chumvichumvi, umami na uchungu.


Kielelezo: Sehemu za ulimi zinazotambua ladha mbalimbali


Sehemu za ulimi na kazi zake

Kila sehemu ya ulimi ina uwezo wa kutambua zaidi ladha ya aina fulani.

Jedwali:Sehemu za ulimi na kazi zake

NA

Sehemu ya ulimi

kazi

1

Sehemu ya ncha ya ulimi

Kutambua ladha ya utamu

2

Pande mbili za sehemu ya mbele ya ulimi

Kutambua ladha ya chumvichumvi

3

Sehemu ya kati ya ulimi

Kutambua ladha ya umami

4

Sehemu za pembezoni za ulimi

Kutambua ladha ya uchachu

5

Sehemu ya nyuma ya ulimi

Kutambua ladha ya uchungu

 

Utunzaji wa ulimi

Ili kulinda ulimi wako zingatia yafuatayo:

a)      Safisha kinywa chako mara kwa mara;

b)      Epuka kutumia vyakula vyenye hali ya joto la juu au baridi sana ili kutunza seli onji za ulimi;

c)       Usionje vitu usivyovifahamu kwa sababu vingine vinaweza kuwa na sumu; na

d)      Usitoboe ulimi.

 

Pua

Pua ni ogani yenye matundu mawili iliyopo sehemu ya usoni. Matundu hayo yametenganishwa na mfupa laini. Kazi ya pua ni kunusa na kubaini harufu za vitu mbalimbali. Kazi nyingine ya pua ni kupitisha hewa wakati wa kupumua. Harufu za vitu husafiri katika hewa na kuingia puani. Taarifa za harufu husafirishwa hadi kwenye ubongo kwa ajili ya kutafsiriwa.

 


Kielelezo: pua

Utunzaji wa pua

Tunza pua kwa kufanya yafuatayo:

(a) Safisha pua kwa maji safi na salama; na

(b) Usiingize vitu kwenye matundu ya pua.

 

Ngozi

Ngozi ni ogani inayofunika mwili wa wanyama akiwemo binadamu. Kazi ya ngozi ni kuhisi hali mbalimbali kama vile joto, baridi, mguso, mgandamizo, maumivu, unamu na mitetemo. Ngozi huhisi kwa kupeleka taarifa kwenye ubongo ili itafsiriwe. Ngozi imegawanyika katika matabaka matatu, ambayo ni tabaka la juu, tabaka la kati na tabaka la ndani.

 


Kielelezo: sehemu za Ngozi

 

Utunzaji wa ngozi

Itunze ngozi kwa kufanya yafuatayo:

(a) Safisha ngozi kwa kuoga;

(b) Tumia maji safi, dodoki au brashi na sabuni wakati wa kuoga;

(c) Kausha mwili wako kwa kutumia taulo safi baada ya kuoga;

(d) Paka mafuta sahihi ya ngozi baada ya kuoga; na

(e) Kula vyakula bora na kunywa maji ya kutosha.

 

 

 

Sikio

Sikio ni ogani inayotuwezesha kusikia na kutambua sauti. Sikio limegawanyika katika sehemu kuu tatu. Sehemu hizo ni sehemu ya nje, sehemu ya kati na sehemu ya ndani.

 


Kielelezo:sehemu za sikio

 

Kutambua sauti

Sehemu ya nje ya sikio hukusanya mawimbi ya sauti. Pia, huyaelekeza mawimbi hayo katika sehemu ya kati ya sikio kupitia kwenye ngoma ya sikio. Sehemu ya kati ya sikio hupokea mawimbi ya sauti kutoka kwenye ngoma ya sikio na kuyapitisha hadi sehemu ya ndani ya sikio. Sehemu ya ndani ya sikio husafirisha mawimbi ya sauti mpaka kwenye ubongo ili yatafsiriwe kama sauti.

Utunzaji wa masikio

Tunapaswa kutunza masikio ili kuepuka athari zinazoweza kuathiri uwezo wa kusikia. Mambo muhimu ya kuzingatia ni:

(a) Kutosikiliza sauti za juu. Mfano, kutosikiliza sauti ya juu ya redio au runinga;

(b) Kutoingiza vitu vyenye ncha kali au vilivyochongoka katika masikio kwani vinaweza kutoboa ngoma ya sikio;

(c) Unapooga au kuogelea hakikisha maji hayaingii sehemu za ndani za masikio;

(d) Usitoe nta ya ndani ya sikio. Nta husaidia kuzuia vitu mbalimbali kama vile vumbi na vimelea vya magonjwa kuingia ndani ya sikio; na

(e) Muone daktari wa masikio pale inapobidi kwa ajili ya uchunguzi.


Umuhimu wa milango ya fahamu

Milango ya fahamu ni muhimu katika mwili wa binadamu. Husaidia kujifunza, kuyatambua mazingira yetu na kuchukua hatua stahiki. Athari yoyote katika milango ya fahamu, huathiri tafsiri ya vichocheo vitokavyo kwenye mazingira. Kwa mfano, kasoro kwenye sikio huweza kusababisha mtu awe kiziwi na kasoro kwenye macho huweza kusababisha mtu asiweze kuona




Sura ya tatu: Viumbehai na vitu visivyo hai

Viumbehai na vitu visivyo hai katika mazingira

Mazingira yameundwa na viumbehai na vitu visivyo hai. Mifano ya viumbehai ni wanyama na mimea. Vitu visivyo hai ni kama vile jiwe, gari, mlima na nyumba.

Sifa za viumbehai

Viumbehai wana sifa kuu saba, ambazo ni kula, kupumua, kuitikia vichocheo, kujongea, kuzaliana, kutoa takamwili na kukua.

Kula

Viumbehai huhitaji chakula ili waendelee kuishi. Wanyama hula vyakula vinavyotokana na wanyama na mimea.Vyakula huvipatia viumbehai virutubisho mbalimbali kama vile protini, wanga, mafuta, madini na vitamini. Virutubisho huvifanya viumbehai kukua na kupata nguvu. Vilevile, virutubisho husaidia mwili kujikinga na magonjwa mbalimbali. Mimea hujitengenezea chakula kwa kutumia kabonidayoksaidi, maji na uwepo wa mwanga wa jua

Kupumua

Viumbehai vyote hupumua. Wanyama na mimea huingiza gesi ya oksijeni na kutoa gesi ya kabonidayoksaidi wakati wa upumuaji. Upumuaji husaidia kuupatia mwili nguvu kwa ajili ya shughuli mbalimbali. Kuitikia vichocheo Viumbehai huitikia vichocheo kutoka ndani na nje ya mwili. Mfano wa vichocheo ni mwanga, joto, sauti na ladha. Wanyama huitikia vichocheo kwa kutumia milango ya fahamu kama vile pua, ngozi, macho, ulimi na masikio. Mimea huitikia vichocheo kupitia mizizi, shina, matawi, majani na maua.

 


Kielelezo: Kuitikia kichocheo cha mwanga kwa mmea

Kujongea

Viumbehai wote hujongea. Kujongea kunahusisha kusogea kutoka sehemu moja hadi nyingine. Vilevile, kubadili mwelekeo kwa kiumbehai mzima au sehemu ya mwili wa kiumbehai. Wanyama hujongea kwa kutembea, kupaa, kuruka au kutambaa. Mimea hujongea kwa kubadili mwelekeo wa sehemu ya mmea. Mfano wa kujongea kwa mmea ni kwa kupinda au kujizungusha kwenye kitu au mmea mwingine. Mimea hujongea taratibu sana kiasi kwamba ni vigumu kuona mjongeo huo kwa urahisi. Kujongea husaidia viumbehai kupata chakula na kuepuka mazingira hatarishi.


 

Kuzaliana

Uwepo wa viumbehai vyote ni matokeo ya kuzaliana. Kuzaliana ni muhimu kwa mwendelezo wa vizazi. Viumbehai huongezeka idadi kwa njia ya kuzaliana. Wanyama huzaliana kwa njia ya kuzaa watoto hai au kwa kutaga mayai. Mifano ya wanyama wanaozaliana kwa kuzaa watoto hai ni binadamu, mbuzi, popo na paka. Wanyama wanaozaliana kwa kutaga mayai ni kuku, nyoka, mjusi na chura.

Mimea huzaliana kwa kutumia mbegu, mfano mahindi au kuotesha mashina na vipandikizi, mfano mihogo.

 

Kutoa takamwili

Viumbehai hutoa takamwili katika hali ya gesi na majimaji. Wanyama hutoa maji ya ziada na chumvichumvi nje ya mwili kwa njia ya mkojo na jasho. Pia, hutoa gesi kwa njia ya kupumua. Mimea hutoa takamwili katika hali ya maji, gesi na utomvu. Takamwili hizi hutolewa kupitia majani, shina au mizizi.

Kukua

Viumbehai wote hukua. Wanyama akiwemo binadamu hukua kwa kuongezeka kimo na uzito. Wanyama hupitia hatua mbalimbali za ukuaji. Mfano binadamu hukua kutoka utoto, ujana, utu uzima hadi uzee. Mimea hupitia hatua mbalimbali za ukuaji kwa kuongezeka kimo na uzito. Ukipanda mbegu baada ya muda itaota na kuwa mche. Kisha mche utakua na kuwa mmea kamili

 


Kielelezo: ukuaji wa mmea

Makundi makuu ya viumbehai

Katika mazingira tunayoishi kuna makundi makuu mawili ya viumbehai. Makundi hayo ni wanyama na mimea.

Wanyama

Wanyama wamegawanyika katika makundi makuu mawili. Wanyama wenye uti wa mgongo na wanyama wasio na uti wa mgongo.

Uti wa mgongo ni muunganiko wa pingili za mifupa inayoanzia kisogoni hadi sehemu ya chini ya kiuno. Kwa wanyama wenye mkia, pingili hizi hushuka hadi mkiani. Uti wa mgongo unasaidia kukinga ugwe mgongo na kuupa mwili umbo. Wanyama wenye uti wa mgongo Wanyama wenye uti wa mgongo wamegawanyika katika makundi matano, ambayo ni samaki, amfibia, reptilia, ndege na mamalia. Mfano wa Wanyama wenye uti wa mgongo ni binadamu, samaki, mjusi, chura na ndege

Samaki

Samaki ni viumbehai wanaoishi ndani ya maji. Kuna kundi la samaki wanaoishi katika majichumvi. Mfano wa samaki hawa ni papa. Samaki wengine kama vile sangara na kambale huishi katika maji baridi.

Sifa za samaki

1. Baadhi ya samaki kama vile sato miili yao imefunikwa kwa magamba. Samaki wengine kama vile kibua na kambale hawana magamba

2. Samaki wanazaliana kwa kutaga mayai.

3. Samaki wana mapezi wanayotumia kuogelea na kubadili mwelekeo na mwendo.

4. Umbile la samaki limechongoka kwa upande wa mbele ili kumsaidia kujongea kwa urahisi ndani ya maji.

5. Juu ya mwili wa samaki kuna ute unaozuia vimelea vya magonjwa kuingia mwilini.

6. Samaki wanatumia matamvua kwa ajili ya kupumua.

7. Joto la miili ya samaki hubadilika kulingana na joto la mazingira.

 

Amfibia

Ni wanyama wenye uti wa mgongo. Amfibia huishi majini katika hatua za awali za ukuaji. Mfano wa wanyama katika kundi hili ni chura.

Sifa za amfibia

1. Amfibia wengi wana miguu minne; miguu ya mbele ni mifupi na miguu ya nyuma ni mirefu.

2. Amfibia wana ngozi laini yenye unyevunyevu.

3. Amfibia wana matamvua katika hatua za awali za ukuaji, yaani lava na huwasadia katika upumuaji. Wakikua hutumia mapafu na ngozi.

4. Amfibia hutaga mayai ndani ya maji.

5. Amfibia wana ulimi mrefu unaotumika kudaka wadudu kwa urahisi.

6. Joto la miili ya amfibia hubadilika kulingana na joto la mazingira.

 

Reptilia

Kundi hili linajumuisha wanyama wanaoishi nchi kavu na wanaoishi kwenye maji. Mifano ya reptilia wanaoishi nchi kavu ni kinyonga, mjusi, kobe na nyoka. Mifano ya reptilia wanaoishi majini na nchi kavu ni mamba, kasa, kenge na baadhi ya nyoka.


 

Sifa za reptilia

1. Ngozi ya reptilia ni kavu na imefunikwa na magamba magumu.

2. Reptilia huzaa kwa kutaga mayai nchi kavu.

3. Reptilia hujongea kwa kutumia miguu. Baadhi yao, kwa mfano nyoka, hawana miguu. Hawa hujongea kwa kutambaa. 4. Hutumia mapafu kwa ajili ya kupumua.

5. Joto la miili ya reptilia hubadilika kulingana na joto la mazingira.

 

Ndege

Ndege ni wanyama wenye uti wa mgongo na manyoya. Baadhi ya ndege hufugwa na wengine huishi porini. Mifano ya ndege wafugwao ni kuku, bata, njiwa, kanga, tausi na kasuku. Mifano ya ndege waishio porini ni mwewe, bundi, kwale, kunguru na mbuni. Ndege wengi huishi nchi kavu, ila baadhi yao huishi kwenye maji.

Sifa za ndege

1. Mwili wa ndege umechongoka nyuma na mbele. Umbo hilo humsaidia kupaa hewani kwa urahisi.

2. Mwili wa ndege umefunikwa kwa manyoya ambayo humsaidia kuhifadhi joto la mwili.

3. Ndege wana mabawa yanayomwezesha kupaa hewani.

4. Ndege wana mdomo mgumu, umechongoka na hauna meno.

5. Ndege huzaa kwa kutaga mayai.

6. Ndege wana miguu miwili iliyofunikwa kwa magamba.

7. Joto la miili ya ndege halibadiliki kulingana na joto la mazingira.

 

Mamalia

Mamalia ni wanyama wenye viwele. Viwele vya mamalia wa kike hutoa maziwa kwa ajili ya watoto kunyonya. Mifano ya mamalia ni binadamu, popo, nyangumi, panya, tembo, mbwa, punda, simba, farasi, pundamilia, chui, kangaruu, ng’ombe, mbuzi,nyani na kondoo

Sifa za mamalia

1. Mamalia wote wana viwele. Kwa mamalia wa kike viwele hivyo huzalisha maziwa kwa ajili ya kuwanyonyesha watoto wao.

2. Miili ya mamalia imefunikwa na vinyweleo vinavyowasaidia kutunza joto la mwili.

3. Ngozi ya mamalia ina tezi za jasho.

4. Mamalia huzaa watoto walio hai na waliokamilika mfano, binadamu na ng’ombe.

5. Mamalia walio wengi huishi nchi kavu na baadhi yao huishi kwenye maji. Mifano ya mamalia waishio kwenye maji ni nyangumi na pomboo.

6. Mamalia wana damu moto.

7. Mamalia wanatumia mapafu kupumua.

8. Mamalia wana masikio ya nje.

 

Wanyama wasio na uti wa mgongo

Mifano ya wanyama wasio na uti wa mgongo ni konokono, nyungunyungu na panzi.

 

Mimea

Katika mazingira tunayoishi kuna mimea ya aina mbalimbali. Mimea inatofautiana kwa ukubwa, muundo na makazi. Baadhi ya mimea hukua na kustawi kwenye maji. Mfano wa mimea inayoota kwenye maji ni magugu maji. Vilevile, mimea mingine hukua na kustawi nchi kavu. Baadhi ya mimea hiyo ni mbuyu na mpapai

Sehemu za mmea

Mmea una sehemu kuu tatu, ambazo ni mizizi, shina na majani. Sehemu hizo zina kazi mbalimbali ambazo zinawezesha mmea kukua vizuri.

 


Kielelezo: sehemeu za mmea

Mizizi

Kazi kuu ya mizizi ni kufyonza maji na virutubisho kutoka kwenye udongo. Pia, mizizi hushikilia mmea kwenye udongo ili usianguke. Vilevile, mizizi huhifadhi chakula kwa baadhi ya mimea. Mifano ya mimea inayohifadhi chakula kwenye mizizi ni karoti, mihogo na viazi vitamu


Shina

Kazi ya shina ni kushikilia majani, maua na matunda. Kazi nyingine ya shina ni kusafirisha maji, virutubisho na madini kutoka kwenye mizizi kwenda kwenye matawi na majani. Baadhi ya mimea inahifadhi chakula kwenye mashina.Mimea hiyo ni pamoja na nanasi, vitunguu na miwa.


Majani

Kazi ya majani ni kutengeneza chakula cha mmea. Majani ya mimea yana vitundu vidogo vinavyoitwa stomata. Stomata hufunga na hufunguka ili kudhibiti kiwango cha maji katika mmea. Pia, huruhusu gesi ya oksijeni na kabonidayoksaidi kuingia na kutoka kwenye mmea.

Mimea imegawanyika katika makundi makuu mawili ambayo ni mimea inayotoa maua na mimea isiyotoa maua.

Mimea inayotoa maua

Hii ni mimea inayotoa maua na matunda. Mifano ya mimea hiyo ni ngano, maharage, miembe, njegere, mpunga, alizeti, uaridi na mahindi. Ua hubadilika kuwa tunda. Tunda hutoa mbegu zinazoota na kuwa mche. Mche hukua na kuwa mmea kamili. Sehemu za ua ni pamoja na petali, sepali na kikonyo.

 


Kielelezo: sehemu za ua

 

Mimea isiyotoa maua

Baadhi ya mimea haitoi maua lakini inatoa mbegu. Mbegu za mimea hii hazifunikwi ndani ya tunda, kwa mfano mvinje na mfeni.

 

Kutegemeana kwa viumbehai

Viumbehai wanategemeana kwa namna mbalimbali katika mazingira yao. Mimea na wanyama hutegemeana kwa chakula, makazi na hewa. Mimea inaweza kujitengenezea chakula chake yenyewe. Hii ndio sababu mimea ni chanzo kikuu cha chakula kwa wanyama walio wengi. Mimea huzalisha gesi ya oksijeni wakati wa usanishaji wa chakula. Gesi hii hutumiwa na wanyama pamoja na mimea yenyewe katika upumuaji. Vilevile, mimea nayo hutegemea gesi ya kabonidayoksaidi inayotoka kwa wanyama wakati wa upumuaji ili kujitengenezea chakula chake.

 

Kutunza viumbehai

Viumbehai wote wanahitaji kutunzwa kwa kuwapatia mahitaji yao. Mahitaji hayo ni pamoja na; hewa, chakula, mwanga na maji. Utunzaji wa viumbehai huwawezesha kuzaliana, kukua na kuishi. Kwa mfano, wanyama wanahitaji kukaa sehemu salama yenye chakula, maji na hewa. Vilevile, mimea huhitaji sehemu yenye mwanga, maji, hewa na virutubisho ili iweze kukua




Sura ya nne: uchunguzi wa kisayansi

Maana ya uchunguzi wa kisayansi

Uchunguzi wa kisayansi ni kitendo cha kutafuta majibu ya maswali kwa kutumia mbinu mbalimbali za kiutafiti. Utafiti unahusisha kutafuta taarifa kwa lengo la kujenga maarifa mapya au kuboresha maarifa yaliyopo. Uchunguzi wa kisayansi hutumia njia za kisayansi kutafuta majibu ya maswali. Vilevile, uchunguzi wa kisayansi hufuata hatua zenye mpangilio maalumu.

 

Sababu za kufanya uchunguzi wa kisayansi

Uchunguzi wa kisayansi hufanywa kwa sababu maalumu. Baadhi ya sababu za kufanya uchunguzi wa kisayansi zinaweza kuwa: Kutafuta majibu ya maswali ya kisayansi, kutafuta maarifa au mawazo mapya, kuthibitisha au kukanusha kanuni za kisayansi, kuthibitisha dhanio au kufafanua matukio ya asili.

Mahitaji ya kufanyia uchunguzi wa kisayansi

Uchunguzi wa kisayansi unahitaji mahitaji mbalimbali ili uweze kufanyika. Mahitaji hutegemea aina ya uchunguzi husika. Miongoni mwa mahitaji ya kufanyia uchunguzi ni kama yafuatayo:

(a) Viumbehai, yaani mimea au sehemu ya mimea kama vile majani, shina, mbegu, mizizi au maua. Pia, wanyama au sehemu ya wanyama kama vile nyama, mifupa na nywele.

(b) Vitu visivyo hai, kama vile udongo, mawe, maji, tindikali, chumvi na nyongo.

(c) Vifaa mbalimbali, kama vile vifaa vya kupimia mfano futikamba, mizani, saa, kipimajoto na bika. Pia, kuna vifaa kwa ajili ya kuchunguza viumbehai na vitu vidogo. Mfano wa vifaa hivyo ni kama vile lenzi ya mkononi na hadubini. Vilevile, vifaa vya kuhifadhia sampuli mfano mifuko ya plastiki, chupa, makasha na jokofu.

(d) Vifaa vya kurekodia data wakati wa uchunguzi wa kisayansi kama vile daftari, kalamu, kalamu rashasha na penseli.


Hatua za kufanya uchunguzi wa kisayansi

Uchunguzi wa kisayansi hufanyika kwa kufuata hatua zenye mpangilio maalumu


Kielelezo: hatua za kufanya uchunguzi wa kisayansi

Hatua za kufanya uchunguzi wa kisayansi zinaelezewa kama ifuatavyo:

1. Kubaini tatizo

Hatua ya kwanza ya uchunguzi wa kisayansi ni kubaini tatizo au jambo linalohitaji kupatiwa ufumbuzi au jibu. Kwa mfano, kutofautiana kwa ukuaji wa mchicha kati ya bustani mbili linaweza kuwa tatizo linalohitaji majibu kupitia uchunguzi wa kisayansi.

2. Kubuni dhanio

Dhanio ni utabiri wa matokeo ya kubuni kuhusu tatizo fulani. Katika hatua hii unaweza kujiuliza, Je, ni kitu gani kinaweza kusababisha tatizo ulilolibaini? Au ni jibu lipi linaweza kujibu swali lililopo? Kwa mfano, katika jaribio letu, dhanio linaweza kuwa ukuaji wa mchicha unaathiriwa na kiwango cha maji. Umuhimu wa hatua hii inakusaidia kufanya uchunguzi utakaopelekea kukubali au kukataa dhanio. Iwapo dhanio halikuweza kujibu swali lako, unarudi kujaribisha dhanio lingine.

3. Kuandaa mahitaji ya jaribio

Hatua hii inahusisha kuandaa vifaa ambavyo vitatumika katika kufanya jaribio. Pia, kuandaa sehemu au mazingira yanayofaa kufanyia jaribio hilo. Hatua hii ni muhimu katika kufanya jaribio. Kutokuwa na mahitaji muhimu kutasababisha jaribio lako kutofanikiwa. Hali hiyo itasababisha kukosa data sahihi. Mfano wa vifaa vitakavyotumika katika jaribio hili ni jembe na ndoo yenye maji. Mahitaji mengine ni mbegu na mbolea. Pia, eneo lenye mwanga na udongo wenye rutuba ya kutosha.

4. Kufanya jaribio na kukusanya data

Hatua hii inahusisha kufanya jaribio kwa kutumia vifaa vilivyoandaliwa. Kwa mfano, katika jaribio letu unaweza kuotesha mbegu katika bustani mbili. Baada ya mbegu kuota bustani moja utaimwagilia maji asubuhi na jioni na bustani nyingine usiimwagilie. Pia, hatua hii hujumuisha ukusanyaji wa data zilizopatikana wakati wa kufanya jaribio. Data hutokana na hatua au njia ulizofuata wakati wa kufanya jaribio. Unaweza kupima urefu wa mchicha kila baada ya siku mbili ili kujua unaokua haraka zaidi. Ni vyema kuwa makini wakati wa kufanya jaribio na kukusanya data.

5. Kuchambua data

Hatua hii huhusisha kuzipanga data, kuzichambua na kuziweka katika utaratibu mzuri. Kwa mfano katika jaribio letu, data zikishakusanywa kutoka kwenye majaribio yote zinapaswa kuchambuliwa vizuri. Unaweza kupanga na kulinganisha urefu wa mchicha kati ya bustani iliyomwagiliwa na isiyo mwagiliwa. Hii itakuwezesha kujua ni mchicha wa bustani gani unakua vizuri zaidi.

6. Kutafsiri matokeo

Kwenye hatua hii data zilizochambuliwa hutafsiriwa na matokeo yake huwekwa kwenye kumbukumbu. Majibu ya uchambuzi wa data huweza kutolewa kwa njia ya maelezo, chati, grafu au jedwali ambayo hurahisisha kutafsiri matokeo. Vilevile, huwasaidia wengine kufahamu kwa urahisi matokeo ya jaribio lililofanywa. Mfano wa jedwali la data ni kama ufuatao:

Jedwali: Athari za maji katika ukuaji wa mchicha

Aina ya bustani

Siku ya 1

Siku ya 3

Siku ya 5

Siku ya 7

Siku ya 9

Matokeo ya ukuaji

Bustani iliyomwagiliwa

sm 1

sm 2

sm 4

sm 6

sm 8

Mchicha umekua vizuri

Bustani isiyomwagiliwa

sm 1

sm 1

sm 1

sm 1

sm 2

Mchicha haujakua vizuri

 

Kutokana na data zilizooneshwa katika jedwali, mchicha uliyomwagiliwa ulikuwa vizuri kuliko usiyo mwagiliwa.

7. Hitimisho

Hatua hii inakuwezesha kuthibitisha au kukanusha dhanio. Pia, kuhusianisha na sababu ya tatizo au swali ulilokuwa umejiuliza. Matokeo ya jaribio yakikubaliana na dhanio, hitimisho litakuwa; “Kuna uhusiano kati ya ukuaji wa mchicha na umwagiliaji wa maji.” Ikiwa matokeo ya jaribio hayakubaliani na dhanio, hitimisho litakuwa; “Hakuna uhusiano kati ya ukuaji wa mchicha na umwagiliaji wa maji.”

8. Kuandika taarifa ya kisayansi

Baada ya jaribio kukamilika kazi inayofuata ni kuandika taarifa ya kisayansi ya jaribio lote. Taarifa hii hujumuisha mambo yote yaliyofanyika kuanzia hatua ya kubaini tatizo hadi hitimisho kwa kufuata mpangilio maalumu




Sura ya tano: michezo sahili ya tehama

Michezo sahili

Dhana za kisayansi zinaweza kuwasilishwa kwa njia ya michezo sahili. Vifaa vya TEHAMA vinaweza kutumika kucheza michezo sahili. Baadhi ya vifaa hivyo ni kama vile kompyuta ya mezani, kompyuta mpakato, tableti na simu.

Faida za kutumia michezo sahili katika kujifunza

Kuna faida nyingi za kutumia michezo sahili katika kujifunza. Faida hizo ni pamoja na:

(a) Kujenga kujiamini na kujifunza kwa furaha;

(b) Kujifunza kwa kujitegemea na kwa kushirikiana;

(c) Kukuza stadi mbalimbali za kufanya maamuzi haraka na kutatua changamoto; na

(d) Kukuza ubunifu na ugunduzi wa kisayansi.

 

Michezo ya TEHAMA

Kuna michezo sahili ya aina mbalimbali. Kila mchezo una lengo na mwongozo wa namna ya kucheza. Baadhi ya michezo inahitaji kanuni katika kucheza. Miongoni mwa michezo utakayojifunza katika ngazi hii ni kama vile mtandao wa njia, usimbaji wa njia, usimbuaji wa njia na mnara wa Hanoi. Katika kujifunza na kucheza michezo hii utatumia programu tumizi inayoitwa “GCompris”. Programu hiyo inaweza kupakuliwa kutoka https://tie.go.tz/ pages/download-software

Post a Comment

Visit Website
Visit Website