Visit Website

Kwa mahitaji ya mitihani, Maazimio ya kazi, Shajara, Notes, na materials mbalimbali ya kielimu, wasiliana nasi ujipatie huduma zetu kwa gharama nafuu sana.

Tunatoa huduma za materials mbalimbali za kielimu kwa gharama nafuu wasiliana nasi leo..

[PDF] Nukuu za somo sanaa na michezo darasa la tatu

Nukuu za somo sanaa na michezo darasa la tatu pdf download | nukuu za somo pdf | notes za sanaa na michezo pdf download | sanaa na michezo free pdf

Nukuu za somo sanaa na michezo darasa la tatu pdf | sanaa na michezo darasa la tatu pdf download | sanaa na michezo pdf download


Sura ya kwanza: Uigizaji

Uigizaji

Kuigiza ni kitendo cha kufuatisha kitu au jambo la mwingine. Uigizaji ni kitendo cha uwasilishaji wa uhalisia wa maisha ya mwanadamu katika mazingira yake. Uigizaji hufanyika.

mbele ya watazamaji ili kufikisha ujumbe uliokusudiwa. Onesho linalofanyika wakati wa kuigiza huitwa igizo. Yapo maigizo ya kutumia maneno na vitendo, maigizo bubu na maigizo ngoma. Igizo humalizika kwa furaha au kwa huzuni. Muigizaji huzingatia matumizi ya miendo ya mwili, muonekano wa sura, sauti, mazingira na ufikirifu. Hii inalenga kuonesha uhalisia wa jambo analoliigiza. Uigizaji unahusisha sifa kuu nne, ambazo ni:

(a) Uwepo wa muigizaji ambaye huitwa fanani;

(b) Uwepo wa ujumbe ambao wakati mwingine huitwa dhamira;

(c) Uwepo wa mahali pa kuigizia ambapo huitwa jukwaa; na

(d) Uwepo wa watazamaji ambao hujulikana kama hadhira.

Ili uweze kuigiza vizuri ni lazima kufanya mazoezi ya kutosha ya sauti na vitendo. Kielelezo namba 1 kinaonesha wanafunzi wakifanya mazoezi ya kuigiza.

Mambo ya kuzingatia katika Uigizaji

Kuna mambo ya kuzingatia katika kuigiza, ambayo ni:

(a) Kuwepo kwa watendaji;

(b) Kuwepo kwa watazamaji;

(c) Kuwepo kwa eneo la kuigizia;

(d) Kutoa sauti inayosikika vizuri;

(e) Kuonesha matendo ya kiishara na mkao wa mwili;

(f) Kutumia vizuri vifaa na maleba;

(g) Kutumia vizuri mapambo;

(h) Kutumia vizuri jukwaa; na

(i) Kutoa ujumbe kwa usahihi.

 

Kuigiza sauti za viumbe hai

Viumbe hai hutumia sauti kuwasiliana katika mazingira yao.

Kuigiza sauti za vitu visivyo na uhai

Katika mazingira yetu tumezungukwa na vitu mbalimbali visivyo na uhai. Mfano wa vitu hivyo ni upepo, maji, gari, jiwe, kiti na meza. Baadhi ya vitu visivyo na uhai hutoa sauti. Sauti hizo zinaweza kuigizwa.


Matumizi ya sauti katika uigizaji

Sauti ni miongoni mwa sifa anazotakiwa kuwa nazo muigizaji. Sauti hutumika katika uigizaji ili:

(a) Maneno ya muigizaji yasikike vizuri;

(b) Kuvutia hadhira kumsikiliza muigizaji;

(c) Kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa hadhira kwa uhakika;

(d) Kutambua aina ya muigizaji; na

(e) Kuonesha hisia za muigizaji.


Umuhimu wa Uigizaji

Uigizaji una umuhimu mkubwa katika jamii. Baadhi ya umuhimu huo ni:

(a) Kuburudisha;

(b) Kuelimisha;

(c) Kuingiza kipato;

(d) Kudumisha utamaduni;

(e) Kujenga afya;

(f) Kufikisha ujumbe;

(g) Kujenga stadi ya kuzungumza;

(h) Kujenga hali ya kujiamini;

(i) Kuibua na kuendeleza vipaji; na

(j) Kujenga hali ya ubunifu.





Sura ya pili: Uimbaji

Maana ya uimbaji

Uimbaji ni kitendo cha kutamka maneno katika hali ya kuimbika. Kuna aina mbalimbali za nyimbo zinazoimbwa kwenye mazingira yetu. Mfano wa nyimbo hizi ni ngoma za asili, kwaya, muziki wa dansi, bongo fleva, singeli na taarabu.

Mkao sahihi wakati wa uimbaji

Mkao katika uimbaji ni jinsi mwimbaji anavyojiweka wakati wa kuimba. Mwimbaji anaweza kuimba akiwa amesimama wima, amekaa au anacheza. Mkao sahihi wakati wa uimbaji huuweka mwili katika hali ya usawa na kurahisisha upumuaji. Wakati wote mwimbaji anatakiwa kuhakikisha sehemu mbalimbali za mwili wake zipo kwenye hali au mkao sahihi kama vile:

(a) Shingo kuwa katika hali ya usawa, bila kuinuka au kuinama;

(b) Mabega na mikono kulegezwa;

(c) Kifua na tumbo kutokubana; na

(d) Miguu kuachana kidogo bila kufungana.


Upumuaji sahihi wakati wakuimba

Upumuaji sahihi unamsaidia mwimbaji kuimba bila kukatakata maneno ili kufikisha ujumbe kwa usahihi. Ili kuweza kupumua kwa usahihi wakati wa kuimba, mwimbaji anatakiwa kufanya mazoezi ya pumzi. Kwa mfano, kuvuta hewa na kuitunza kwa muda na kisha kuitoa taratibu. Zoezi hili linamsaidia mwimbaji kuwa na uwezo wa kukusanya hewa ya kutosha wakati wa kuimba. Mwimbaji anapokusanya hewa ya kutosha, inamsaidia kuimba bila kukatakata maneno ya wimbo. Kwa mfano, katika wimbo wa Mungu Ibariki Afrikamwimbaji hatakiwi kupumzika mpaka amalize kutamka maneno yote ya sentensi ya kwanza ya wimbo huu.


Kuimba kwa sauti moja

Nyimbo zinaweza kuimbwa kwa sauti moja, mbili, tatu au nne. Katika hatua hii, utajifunza kuimba kwa sauti moja. Kuimba kwa sauti moja kunahusisha sauti ya kwanza ambayo ndiyo sauti ya msingi ya wimbo husika. Kwa mfano, kwaya ya halaiki ambayo huhusisha uimbaji wa watu wengi, huimba kwa sauti moja.


Umuhimu wa uimbaji

Uimbaji una umuhimu mkubwa katika jamii. Watu hutumia uimbaji katika shughuli mbalimbali kama vile:

(a) Kusaidia katika stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu;

(b) Kuhamasisha watu kufanya kazi, kwa mfano, kulima;

(c) Kufariji jamii, kwa mfano, nyimbo za faraja wakati wa misiba;

(d) Kusifia watu waliofanya mambo mazuri kwenye jamii, kwa mfano, nyimbo za kumsifia kiongozi wa nchi;

(e) Kuburudisha jamii, kwa mfano, nyimbo za sherehe mbalimbali;

(f) Kuonya watu wanaotenda mambo mabaya, kwa mfano, nyimbo katika hadithi;

(g) Kuleta umoja na utambulisho wa kitaifa, kwa mfano, wimbo wa Taifa;

(h) Kutengeneza kipato, kwa mfano, kuuza nyimbo au kulipwa pesa baada ya kuimba katika matukio mbalimbali; na

(i) Kujenga stadi za kuzungumza, kwa mfano, nyimbo za watoto.





Sura ya tatu: Ala za muziki

Maana ya ala za mziki

Ala za muziki ni vifaa vinavyotumika kuzalisha sauti mbalimbali katika muziki. Kila aina ya ala ina sauti yake maalumu inayoweza kufanya muziki kuwa wa kuvutia na wenye ladha na hisia tofauti. Ala hizi zinaweza kuongeza uzuri katika muziki kwa kutoa sauti zinazoendana na sauti za waimbaji au ala nyingine.

Aina za ala za muziki

Ala za muziki zimegawanyika katika makundi mbalimbali. Makundi haya ni kama vile; ala za kupuliza, ala za kugonga, ala za nyuzi na ala za kutikisa. Ala hizi zipo za aina tofauti zinazoweza kupatikana katika jamii mbalimbali duniani.

Ala za kupuliza

Hizi ni aina za ala za muziki ambazo mpigaji anahitaji kupuliza hewa ndani yake ili zitoe sauti. Mfano wa ala hizi ni kama vile tarumbeta, baragumu, filimbi, lipenenga na lilandi. Ala hizi zinaweza kutoa sauti za juu na za chini kwa kutumia njia tofauti za kupuliza.

Kielelezo:Ala za kupuliza


Ala za kugonga

Hizi ni ala ambazo mpigaji anahitaji kuzigonga au kuzipiga ili zitoe sauti. Mpigaji anaweza kutumia mikono au kifaa maalumu kwa ajili ya kupiga ala hizi. Kuna aina nyingi za ala za kugonga. Mfano wa ala hizi ni marimba ya vibao, ngoma, vijiti, chuma cha pembetatu na matoazi.


 





Kielelezo:Ala za kugonga


Ala za nyuzi

Hizi ni ala ambazo sauti zake zinatengenezwa kwa kuvuta au kusugua nyuzi. Mpigaji anaweza kutumia vidole au vifaa maalumu ili kupiga ala hizi. Mfano wa ala hizi ni kama vile gitaa, fidla, kinubi, zeze, enanga, ndono na litungu.






 

Kielelezo:Ala za nyuzi

Ala za kutikisa

Hizi ni ala ambazo hutikiswa ili kutoa sauti. Sauti hizi hutokana na mgongano wa vitu mbalimbali vilivyotumika kutengeneza ala hizi. Mfano wa ala hizi ni manyanga, kayamba na njuga. Ala hizi huwekewa mbegu za nafaka kama vile mahindi au maharage, au mawe madogo madogo ndani yake. Pindi ala hizi zinapotikiswa, mbegu za nafaka au mawe yaliyomo ndani yake hutikisika na kutoa sauti.


  Kielelezo:Ala za kutikisa


Baadhi ya ala za muziki za kutikisa zinaweza kutengenezwa kwa kutumia vifaa vinavyopatikana kwa urahisi kwenye mazingira yetu. Kwa mfano, unaweza kutengeneza manyanga kwa kutumia kipande cha mti chenye matawi pacha, uzi au waya na vifuniko vya soda.

Kielelezo:Ala ya kutikisa

Umuhimu wa ala za muziki

Ala kwenye muziki hupendezesha nyimbo na kuchangamsha uimbaji. Pia, huwaongoza waimbaji kufuata mdundo sahihi na kuimba kwa ulinganifu.


Sura ya nne: Uchoraji

Maana ya Picha

Picha ni kielelezo cha kitu halisi kinachopatikana kwa kuchorwa, kusanifiwa au kupigwa kwa kamera. Unaweza kuziona picha katika mazingira yako ya nyumbani, shuleni, katika vitabu, majarida, mabango ya matangazo na nguo mbalimbali.

Uchoraji wa picha ni sanaa ya kutengeneza picha kwa kutumia vifaa vya asili au vya kidijitali. Baadhi ya vifaa vya asili ni pamoja na penseli, kalamu za rangi, chaki, brashi, na rangi ya kupaka. Pia, vifaa vya asili vinapatikana kwa njia ya kidijitali.

Kuchora picha kwa kutumia penseli

Kwa anayeanza kujifunza kuchora kwa kutumia penseli huchora kwa uhuru bila kutumia rula au vipimo vyovyote. Kielelezo namba 1 kinaonesha mfano wa picha iliyochorwa kwa uhuru kwa kutumia penseli.

kielelezo:Mfano wa picha iliyochorwa kwa uhuru kwa kutumia penseli

Vifaa vya asili vya kuchorea

Vifuatavyo ni vifaa vya asili ambavyo hutumika kuchora picha kwa kutumia penseli:

(a) Penseli;

(b) Karatasi;

(c) Kifutio;

(d) Meza na stuli;

(e) Kibao cha kuchorea; na

(f) Kibanio cha karatasi.

 

Mambo ya kuzingatia katika uchoraji wa picha kwa kutumia penseli

Mambo yafuatayo ni muhimu kuzingatiwa wakati wa kuchora picha kwa kutumia penseli:

1. Chora picha kwa kuzingatia ujumbe. Chora picha kwa uhuru bila kutumia vipimo vyovyote. Uwezo wako wa kujieleza kwa kutumia mchoro ndiyo kitu muhimu. Usijali usahihi wa mchoro bali zingatia ujumbe unaoelezwa na mchoro wako;

2. Andaa wazo au kitu halisi kitakachochorwa;

3. Zingatia matumizi mbalimbali ya mistari ili kueleza ujumbe au muonekano wa mchoro wako. Usijali uhalisia wa mchoro wako bali zingatia ujumbe au muonekano wa umbo ulilolichora.

4. Anza kuchora kwa kutumia mistari myepesi;

5. Tumia kifutio kwa uangalifu ili usichafue mchoro wako;

6. Usitumie kalamu ya wino kuchorea picha; na

7. Unaweza kuonesha sehemu za mwanga na giza inapowezekana ila siyo

 

Hatua za kuzingatia katika kuchora picha kwa kutumia penseli

Ili kuchora picha yenye maana, hatua zifuatazo zinaweza kufuatwa:

1. Chagua vitu unavyotaka kuvichora;

2. Andaa karatasi na penseli ya kuchorea;

3. Anza kuchora picha ya vitu unavyotaka kuvichora kwa kutumia mistari myepesi;

4. Rekebisha sehemu ambayo umekosea kwa kutumia kifutio; na

5. Koleza mistari ya picha kwa usahihi wa ujumbe na muonekano wa maumbo.

Kumbuka kuchora kwa uhuru bila kutumia vipimo. Muonekano wa umbo unaojieleza ndiyo muhimu

Umuhimu wa uchoraji wa picha

Picha huchorwa kwa lengo la:

(a) Kuuza ili kujipatia kipato;

(b) Kupamba na kupendezesha sehemu mbalimbali;

(c) Kuweka kumbukumbu za matukio;

(d) Kuelimisha na kuburudisha jamii;

(e) Kumjengea mtu kumbukumbu ya muda mrefu; na

(f) Kurahisisha jambo kueleweka


Sura ya tano: Ufinyanzi:

Ufinyanzi

Ufinyanzi ni sanaa inayotumika katika kutengeneza maumbo mbalimbali kwa kutumia udongo wa mfinyanzi.

Vilevile, maumbo kama sanamu yanaweza kutengenezwa kwa kutumia saruji, makaratasi, gundi na udongo bandia. Jamii zinazoishi maeneo yenye asili ya udongo wa mfinyanzi, hufinyanga vyombo mbalimbali. Vyombo hivyo ni kama vile vyungu, mitungi, vikombe, sahani na bakuli. Katika jamii hizi udongo wa mfinyanzi unapatikana zaidi kandokando ya mito, sehemu zenye vichuguu na mabonde.

Zipo njia kuu mbili za kufinyanga kwa kutumia udongo ambazo ni kufinyanga kwa mikono na kufinyanga kwa kutumia mashine. Ili kufinyanga umbo lolote lile kuna vifaa vinavyotumika na hatua kadhaa za kufuata. Sanaa ya ufinyanzi huhitaji vifaa vifuatavyo:

(i) Udongo wa mfinyanzi;

(ii) Maji;

(iii) Ubao;

(iv) Kipande cha karatasi; na

(v) Chekeche.

Njia za kufinyanga kwa udongo wa mfinyanzi

Zipo njia mbalimbali za kufinyanga maumbo ya aina tofauti. Njia hizo ni pamoja na; kufinyafinya, bapa na pindi. Kazi ya kufinyanga inahitaji udongo wa mfinyanzi ambao umeandaliwa vizuri ili kutoa kifani cha udongo kinachofaa kwa matumizi mbalimbali.

Kufinyanga kwa njia ya kufinyafinya

Vitu vinavyoweza kufinyangwa kwa kufinywafinywa ni pamoja na vyungu, vikombe, bakuli, sahani, vifaa vya mche duara na vitu vyenye umbo la ngalawa. Kielelezo namba 1 kinaonesha vyombo vilivyofinyangwa kwa udongo wa mfinyanzi kwa njia ya kufinyafinya.

Kielelezo:Vyombo vilivyofinyangwa kwa njia ya kufinyafinya

 


 

Namna ya kuandaa udongo wa mfinyanzi

Kabla ya kufinyanga unahitaji kuandaa udongo kwa hatua zifuatazo:

1. Ponda udongo mpaka uwe laini;

2. Chekecha udongo ili kuondoa mawe madogo madogo na mabaki mengine kama vile nyasi;

3. Weka maji kidogo kidogo kwenye udongo huku ukiukandakanda mpaka ulainike; na

4. Chagua umbo la kitu unachotaka kufinyanga, kisha anza kufinyanga.

 

Hatua za kufinyanga kwa njia ya kufinyafinya

1. Chagua umbo unalotaka kufinyanga.

2. Chukua udongo wa mfinyanzi kiasi kinachotosha kufinyanga umbo ulilokusudia.

3. Kanda udongo kwa kuchanganya na maji ili kuondoa hewa.

4. Viringisha udongo katikati ya viganja hadi litokee dongetufe.

5. Endapo unafinyanga umbo la mche duara kwa mfano kikombe, bonyeza dongetufe kwa kidole gumba hadi katikati ya donge la udongo.

6. Ongeza tundu kwa kufinyafinya ukuta wa dongetufe kati ya dole gumba na vidole vingine vya mkono mmoja huku ukizungusha dongetufe.

7. Endelea kuminyaminya na kuzungusha dongetufe huku ukichunguza unene wa ukuta uwe linganifu.

8. Sawazisha kifaa na unganisha kiungo chochote kitakachohitajika, mfano, mkono wa kikombe au birika.

9. Weka kivulini umbo ulilofinyanga ili likauke kiasi. Kisha, weka urembo au mapambo kabla ya umbo hilo kukauka kabisa halafu endelea kulianika hadi likauke kabisa.

 

Umuhimu wa kufinyanga

Kufinyanga kuna faida nyingi katika jamii ikiwa ni pamoja na:

(a) Kukuza ubunifu;

(b) Kupata kipato;

(c) Kutengeneza vyombo na mapambo;

(d) Kutunza kumbukumbu;

(e) Kuonesha utamaduni wa jamii; na

(f) Kufikisha ujumbe katika jamii.


Sura ya sita: Mazoezi ya viungo

Mazoezi ya viungo

Binadamu hufanya mazoezi ya viungo kwa mitindo mbalimbali. Mfano wa mazoezi hayo ni kukimbia, kuruka na kusimama kwa mguu mmoja. Mazoezi huweza kufanywa na mtu mmoja mmoja au katika vikundi. Mazoezi hujenga ustadi na ukakamavu, mfano, kwa kufanya mazoezi ya kujisawazisha na wepesi. Baadhi ya mazoezi ya kujisawazisha na wepesi ni kama ifuatavyo:

1. Kisigino kidoleni;

2. Hatua za mzabibu;

3. Ngazi ya wepesi; na

4. Mwendo wa mnyama.

 

Kisigino kidoleni

Hili ni zoezi linalojenga msawazo wa mwili na husaidia uwe tayari kufanya michezo na kazi mbalimbali shuleni na nyumbani.

Hatua za kufuata:

1. Fanya mazoezi ya kuandaa mwili.

2. Simama wima huku miguu ikiwa pamoja.

3. Tawanya mikono kuweka msawazo wa mwili.

4. Weka kisigino cha mguu wa kulia mbele ya kidole cha mguu wa kushoto.

5. Endelea kwa kubadilisha mguu wa kushoto mbele ya kidole cha mguu wa kulia

6. Rudia huku ukisonga mbele.

 

Hatua za mzabibu

Hili ni zoezi linalojenga msawazo wa mwili na husaidia uwe tayari kufanya michezo na kazi mbalimbali shuleni na nyumbani.

Hatua za kufuata:

1. Fanya mazoezi ya kuandaa mwili.

2. Simama wima kisha pishanisha miguu.

3. Huku miguu ikiwa imepishanishwa piga hatua 5 mbele, nyuma, kulia na kushoto.

4. Badilisha mguu uliokuwa mbele uwe nyuma, kisha, rudia hatua hizo walau mara tatu.


 

Ngazi ya wepesi

Fanya kila moja ya mazoezi yafuatayo katika urefu kamili wa ngazi ya wepesi. Kila hatua moja ya mazoezi inapaswa kufanywa mara mbili, ikiongozwa kwa mguu tofauti kila wakati.

1.       Pishanisha kukanyaga kwa mguu mmoja tu kwenye kila sanduku (kushoto, kulia, kushoto, kulia).

Kielelezo:Kukanyaga kwa mguu mmoja mmoja kwenye ngazi ya wepesi

2.       Ruka kwenye kila kisanduku kwa mguu mmoja huku mguu mwingine ukibaki hewani wakati wote.

Kielelezo:Kuruka kwa mguu mmoja mmoja kwenye ngazi ya wepesi

 

3.       Ingiza miguu yote miwili kwenye kila kisanduku kabla ya kusonga kwenye kisanduku kinachofuata. Tanguliza mguu mmoja kila wakati.

Kielelezo:Kukanyaga kwa miguu miwili miwili kwenye ngazi ya wepesi

4.       Geuka upande wa kulia, ingiza miguu yote miwili kwenye kila kisanduku kabla ya kusonga kwenye kisanduku kinachofuata upande upande kwa kutanguliza mguu mmoja kila wakati.

Kielelezo:Kukanyaga kwa kutanguliza mguu mmoja mmoja kwenye ngazi ya wepesi

5.       Weka mguu wako wa kulia kwenye kisanduku cha kwanza. Kisha, weka mguu wa kushoto kwenye kisanduku kinachofuata na toa nje mguu wa kulia kwa wakati mmoja.

Kielelezo:Kukanyaga kwa kupishanisha miguu kwenye ngazi ya wepesi

Mwendo wa mnyama

Hili ni zoezi ambalo washiriki hushindana katika timu kuokota vikaratasi vya rangi yao vilivyomwagwa katika eneo la kuchezea huku wakitembea kwa mwendo wa mnyama. Kwa mfano, sungura hukimbia kwa miguu minne, nyani hutembea kwa kuruka ruka kwa miguu minne na kangaroo hutembea kwa kuruka kwa miguu miwili.

Hatua za kufuata:

1. Fanyeni mazoezi ya kuandaa mwili.

2. Wekeni mipaka kwenye eneo la kuchezea.

3. Gawanyikeni katika timu tatu za watu wasiopungua watano.

4. Kila timu ichukue jina kati ya sungura, nyani na kangaroo.

5. Kila timu ifunge vitambaa vya rangi yao vinavyoendana na rangi ya vikaratasi watakavyookota.

6. Tandaza vikaratasi vya rangi tatu tofauti katika eneo la kuchezea.

7. Anzeni kuokota vikaratasi vya rangi ya timu yenu baada ya amri ya mwongozaji.

8. Kila timu itatembea mwendo wa mnyama wao wakati wa kuokota.

9. Acha kuokota amri ya mwongozaji itakapotolewa.

10. Timu iliyookota vikaratasi vingi ndio mshindi wa awamu hiyo.

11. Timu zibadilishane majina ya wanyama na kucheza tena.

12. Mshindi wa jumla ni timu iliyoshinda awamu nyingi zaidi.


Sura ya saba: Michezo ya asili

michezo ya asili

Michezo ya asili ni michezo ambayo imekua ikichezwa tangu enzi za mababu. Michezo hiyo ni pamoja na rede, kukimbia na chupa kichwani, bao na kukimbia na kijiko.

 

Mchezo wa rede

Rede ni mchezo wa mpira unaochezwa kwa mikono. Mchezo huu huchezwa na wavulana na wasichana. Mpira wa kuchezea rede unapaswa kuwa mwepesi. Vilevile, hautakiwi kuwa mkubwa sana. Kuna aina mbalimbali za mchezo wa rede zikiwemo:

1. Rede ya kupanga vigae au vibao; na

2. Rede ya kujaza mchanga kwenye chupa

 

Rede ya kupanga vigae au vibao

Jinsi ya kucheza mchezo huu:

(i) Kuwe na wachezaji watatu. Wa kwanza upande kwa kulia. Wa pili upande wa kushoto. Wa tatu anatakiwa awe katikati ya wachezaji wawili pamoja na vigae au vibao;

(ii) Mchezaji wa upande wa kwanza arushe mpira kwa mchezaji wa upande wa pili;

(iii) Mchezaji wa upande wa pili arushe mpira kwa mchezaji wa upande wa kwanza;

(iv) Mchezaji wa upande wa kwanza atarusha mpira kwa mchezaji wa upande wa pili akimlenga mchezaji wa katikati;

(v) Mpira ukirushwa, mchezaji wa katikati aukwepe. Huku akipanga vigae kimojakimoja kwa wima;

(vi) Mchezaji wa katikati akidaka mpira arushe mbali. Kurusha mbali kutampatia muda wa kupanga vigae vingi zaidi;

(vii) Mchezaji wa katikati aendelee kukwepa na kupanga vigae kimojakimoja kwa wima. Zoezi hili liendelee hadi akipigwa na mpira na kutoka au akimaliza kupanga bila kupigwa na mpira;

(viii) Akipanga vigae vyote bila kupigwa na mpira, atakuwa mshindi;

(ix) Akipigwa na mpira kabla ya kupanga vigae vyote atakuwa ameshindwa. Hivyo, ataingia yule aliyempiga; na

(x) Mchezo huu huchezwa kwa kupokezana.

 

Rede ya kujaza mchanga kwenye chupa

Jinsi ya kucheza mchezo huu:

(i) Kuwe na wachezaji wawili wa kurusha mpira. Mmoja asimame upande wa kulia na mwingine kushoto;

(ii) Mchezaji wa tatu awe katikati yao. Chupa na mchanga uliokusanywa vyote viwe katikati;

(iii) Mpira ukirushwa kutoka upande mmoja kwenda upande wa pili utamlenga mchezaji wa katikati ambaye atatakiwa kuukwepa. Lengo ni aweze kujaza mchanga kwenye chupa;

(iv) Mchezaji wa katikati akiudaka mpira, ataurusha mbali. Kurusha mbali kutampa muda wa kujaza mchanga hadi chupa ijae;

(v) Akijaza bila kupigwa na mpira atakuwa ameshinda;

(vi) Akipigwa na mpira kabla chupa haijajaa mchanga atakuwa ameshindwa. Inabidi atoke na aingie mwingine kucheza; na

(vii) Mchezo huu huchezwa kwa kupokezana.

 

Umuhimu wa mchezo wa rede

Mchezo huu wa rede una umuhimu kwa wachezaji kama vile:

1. Kuuchangamsha mwili;

2. Kujenga urafiki na ushirikiano;

3. Kukuza stadi za kuhesabu;

4. Kuongeza uwezo wa kufikiri;

5. Kuupa mwili mazoezi ya viungo;

6. Kujenga ari ya kushindana; na

7. Kukuza stadi ya kuzungumza.

 

Kukimbia na chupa kichwani

Huu ni mchezo wa asili ambao washiriki hushindana kukimbia wakiwa na chupa kichwani. Mchezo huu hufurahisha na kujenga ushindani. Pia mchezo huu husaidia kuimarisha msawazo wa mwilI.

Namna ya kucheza:

1. Fanya mazoezi ya kuandaa mwili.

2. Weka alama ya kuanzia na kuishia kwenye eneo la kuchezea.

3. Simama kwenye alama ya kuanzia.

4. Weka chupa kichwani, iachie isimame yenyewe

5. Subiri amri ya mwongozaji.

6. Anza kukimbia bila kushikilia chupa baada ya amri ya kuondoka.

7. Kimbia kwa kasi kuwashinda wengine bila kudondosha chupa

8. Mshindi ni yule atakayekuwa wa kwanza kuvuka alama ya kuishia bila kudondosha chupa.

Kukimbia na kijiko

Huu ni mchezo wa asili ambao washiriki hushindana kukimbia wakiwa na kijiko chenye limao au yai. Kijiko kinaweza kushikwa mkononi au kuwekwa mdomoni. Mchezo huu hufurahisha na kujenga ushindani. Pia, mchezo huu husaidia kuimarisha msawazo na wepesi wa mwili.

Vifaa:Kijiko na limao au yai.

Namna ya kucheza:

1. Fanya mazoezi ya kuandaa mwili.

2. Weka alama ya kuanzia na kuishia kwenye eneo la kuchezea.

3. Simama kwenye alama ya kuanzia.

4. Shika kijiko mkononi kisha weka limao au yai juu yake.

5. Subiri amri ya mwongozaji.

6. Baada ya amri ya kuondoka kimbia bila kushikilia yai au limao.

7. Kimbia kwa kasi kuwashinda wengine bila kudondosha limao au yai.

8. Mshindi ni yule atakayekuwa wa kwanza kuvuka alama ya kuishia bila kudondosha limao au yai.


Sura ya nane: Kushiriki maonesho ya sanaa na mashindano ya michezo

Maonesho ya sanaa na mashindano ya michezo

Maonesho ya sanaa pamoja na mashindano ya michezo ni njia nzuri ya kuibua na kukuza kipaji, ubunifu na kujenga ari ya kujiamini kwa mwanafunzi. Katika sura hii, utapata nafasi ya kuonesha kazi mbalimbali za sanaa ulizofanya. Pia, utapata nafasi ya kushiriki mashindano ya michezo kwa ngazi ya darasa. Maonesho ya sanaa yatahusisha kazi za uigizaji, uimbaji, uchoraji na ufinyanzi. Mashindano ya michezo yatajumuisha mazoezi ya viungo na michezo ya asili.

Kushiriki sanaa za maonesho

Ili kushiriki katika sanaa za maonesho, ni vema kuzingatia hatua zifuatazo:

1. Chagua mada kwa ajili ya onesho; ni vyema kuchagua ujumbe ambao unagusa maisha kwenye jamii unayotoka. Mifano ya ujumbe unaoweza kutumika ni rushwa, magonjwa, mazingira, elimu ya kodi na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar;

2. Jiunge katika kikundi na wenzako ili kufanya maandalizi kwa pamoja;

3. Andaeni tangazo la onesho pamoja na ratiba ya maandalizi na hakikisha kuwa ratiba inaonesha muda wa matayarisho, mazoezi na onesho lenyewe;

4. Fanyeni mazoezi ya onesho kwa kuzingatia maelekezo kutoka kwa mwalimu. Hakikisha mnafanya mazoezi ya kutosha ili kuwa na onesho zuri;

5. Andaeni vifaa vinavyohitajika kwenye onesho lenu. Vifaa hivi ni pamoja na mavazi, mapambo na zana mbalimbali kulingana na onesho husika;

6. Fanyeni mazoezi ya onesho katika eneo litakalotumika siku ya onesho;

7. Siku ya onesho hakikisheni kuwa kila kitu kimeandaliwa vizuri hasa jukwaa na vifaa;

8. Kama kuna vifaa vya kielektroniki na vya umeme vifanyiwe majaribio mapema kuona kama viko sawa. Hatua hii ifanyike chini ya usimamizi wa mwalimu;

9. Baada ya onesho, hakikisha eneo lililotumika kuigizia linabaki safi na vifaa vyote vilivyotumika vimeondolewa; na

10. Fanyeni tathmini kubaini ufanisi au mapungufu ya onesho. Hii itasaidia kuboresha maonesho mengine yatakayoandaliwa.

 

Maonesho ya sanaa sanifu

Maonesho ya sanaa sanifu yanamwezesha mwanafunzi kuona ubora wa kazi za wenzake. Hii huhamasisha ari ya kuongeza bidii ya kujifunza. Vilevile, wazazi na jamii kwa ujumla wanapata nafasi ya kuona maendeleo ya watoto wao.

Ili kushiriki katika maonesho ya sanaa sanifu ni vyema kuzingatia hatua zifuatazo:

1. Chagua jina la onesho litakaloendana na kazi za sanaa sanifu; ni vyema kuchagua jina ambalo linagusa maisha kwenye jamii unayotoka.

2. Fanya maandalizi na wenzako kwa pamoja ili kuibua mbinu za kutayarisha onesho lenu kwa ubora wenye mvuto.

3. Tayarisha ratiba fupi ya maandalizi itakayoonesha

(a) Utafutaji wa eneo la maonesho, kama vile darasani;

(b) Utambuzi na utayarishaji wa kazi za sanaa zitakazooneshwa;

(c) Mpangilio na uwekaji wa kazi za sanaa ndani ya eneo la maonesho; na

(d) Tarehe ya kufanyika kwa onesho.

4. Tayarisha vifaa vya kutumika kuandaa onesho. Baadhi ya vifaa hivyo ni

(a) Misumari midogo;

(b) Gundi;

(c) Meza; na

(d) Pini za kubandikia picha.

5. Tayarisha orodha ya kazi za sanaa zilizochaguliwa kuoneshwa

(a) Chagua kazi katika uwiano mzuri ili upate nafasi ya kuonesha kazi zako;

(b) Weka kumbukumbu nzuri ya kazi zilizochaguliwa; na

(c) Chagua mchanganyiko wa picha na maumbo ya kufinyanga katika uwiano mzuri.

6. Tundika au weka kazi za sanaa katika eneo la kuzionesha.

7. Shiriki katika onesho kwa kuwaelekeza watakao tazama kazi hizo.

8. Mwisho wa onesho kusanya kazi za sanaa na safisha eneo ili libaki safi.

 

Maonesho ya uimbaji

Maonesho ya uimbaji ni tukio ambapo waimbaji wanapata fursa ya kuonesha uwezo wao wa kuimba mbele ya hadhira. Maonesho haya hufanyika kwenye majukwaa maalumu au maeneo kama vile shule, kumbi za matamasha au nyumba za sanaa. Watu wanaojumuika katika maonesho haya wanaweza kuwa watoto au watu wazima. Katika maonesho haya, waimbaji hupanda jukwaani na kuimba nyimbo mbalimbali. Waimbaji hulenga kuelimisha, kuburudisha na kufikisha ujumbe fulani kwa hadhira. Maonesho ya uimbaji yanaweza kuhusisha mashindano ya uimbaji au matamasha. Lengo la mashindano au matamasha ni kujipima, kuimarisha uwezo wa uimbaji na kuburudisha. Waimbaji wanaweza kuimba nyimbo zao au nyimbo maalumu zilizopangwa tayari. Pia, wanaweza kuimba kama kikundi au mwimbaji mmoja mmoja. Watu wengi hupenda kuhudhuria maonesho haya ili kufurahia sauti nzuri za waimbaji na ala za muziki. Pia, hufurahia ujumbe wa nyimbo mbalimbali.

Mambo ya kuzingatia wakati wa kushiriki maonesho ya uimbaji

Wakati wa kushiriki katika maonesho ya uimbaji ni vema kuzingatia mambo yafuatayo:

1. Chagua wimbo kwa ajili ya onesho.

Ni vema kuchagua wimbo unaoupenda na wenye ujumbe na mvuto ambao unagusa maisha ya watu kwenye jamii unayotoka;

 

2. Tenga muda wa kutosha wa kufanya mazoezi.

Mazoezi haya yahusishe mazoezi ya sauti na namna wimbo utakavyoimbwa. Kama ni wimbo utakaoimbwa na kikundi, kaa na wenzako ili kufanya maandalizi kwa pamoja. Maandalizi mazuri yanamfanya mwimbaji awe na ujasiri na hivyo kufanya vizuri mbele ya hadhira;

3. Kabla ya onesho, fika katika eneo au jukwaa litakalotumika na kufanya ujaribishaji wa muda mfupi wa namna utakavyoimba siku ya onesho. Ujaribishaji huu ni pamoja na kulifahamu jukwaa na kujaribisha utendaji kazi wa ala za muziki zitakazotumika;

4. Siku ya onesho, tenga muda wa kutosha wa kupumzika kabla ya muda wa onesho.

Hakikisha unafika mapema katika eneo ambapo onesho litafanyika; na

5. Wakati wa onesho la uimbaji, wasilisha hisia za wimbo kwa kujiamini ili kufikisha ujumbe uliokusudiwa.

Ikiwa ni wimbo wa furaha, tabasamu na kuonesha furaha yako. Ikiwa ni wimbo wenye hisia za huzuni, onesha hisia hizo kwa sauti au matendo ya kuigiza.

 

Kushiriki katika mashindano ya michezo

Katika kushiriki mashindano ya michezo unatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:

1. Kufanya mazoezi ya kuandaa mwili kabla ya kushiriki mchezo husika;

2. Kuandaa vifaa vya mchezo husika;

3. Kuvaa nguo za mchezo husika;

4. Kuvaa raba za mchezo husika;

5. Kufanya mazoezi ya kuboresha kiwango cha uchezaji wa mchezo husika;

6. Kucheza kwa kuzingatia sheria za mchezo husika;

7. Kutowachezea wengine vibaya; na

8. Kuepuka ugomvi.

Post a Comment

Visit Website
Visit Website