Nukuu za somo jiografia na mazingira darasa la tatu pdf download | nukuu za somo pdf download | jiografia na mazingira darasa la tatu pdf
Sura ya 01 : Dhana ya Jiografia na Mazingira
Utangulizi Binadamu anapaswa kuielewa Jiografia na kuyafahamu vema mazingira yanayomzunguka ili kujua namna bora ya kuhusiana nayo. Jiografia inamwezesha binadamu kuyaelewa mazingira yanayomzunguka, jinsi ya kuyatumia na kuyahifadhi sasa na kwa vizazi vijavyo. Katika sura hii, utajifunza kuhusu maana ya Jiografia na Mazingira, uhusiano baina ya Jiografia na Mazingira, na umuhimu wa kujifunza Jiografia na Mazingira. Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kuthamini somo la Jiografia na Mazingira. |
Fikiri
Vitu vinavyomzunguka binadamu
Maana ya Jiografia
Jiografia ni somo linalohusu binadamu na mazingira yake. Hivyo, Jiografia inahusu dunia, angahewa, na vitu vilivyopo juu ya uso wa dunia, mtawanyiko wake na jinsi vinavyohusiana na binadamu. Uso wa dunia una mandhari kuu mbili ambazo ni mabara, na bahari. Mandhari hizi zinahusisha maumbo mbalimbali ambayo ni sehemu ya mazingira. Jiografia imejikita katika kumwezesha binadamu kujenga stadi za msingi zitakazomwezesha kuyafahamu mazingira yake na kuhusiana nayo kwa njia endelevu. Kielelezo namba 1 kinaonesha mandhari ya uso wa dunia.
Kielelezo namba 1: Mandhari ya uso wa dunia
|
Maana ya mazingira
Binadamu anavyoishi juu ya uso wa dunia anazungukwa na vitu mbalimbali. Vitu hivi vyote pamoja na binadamu mwenyewe ni sehemu ya mazingira. Hivyo, mazingira ni vitu vyote vinavyomzunguka binadamu. Vitu vinavyomzunguka binadamu vinaweza kuwa ni vya asili ambavyo huunda mazingira ya asili au vilivyotengenezwa na binadamu. Vitu vya asili ni vile ambavyo havijatengenezwa na binadamu kama vile milima, mabonde, misitu, wanyama, mito, bahari, ardhi, na hewa. Vitu vilivyotengenezwa na binadamu ni kama vile nyumba, barabara, bustani, meza, magari na vitu vingine vyote ambavyo siyo vya asili. Maelezo kuhusu vitu vinavyounda mazingira yanaweza kufupishwa kama inavyoonekana katika Kielelezo namba 2.
Kielelezo namba 2: Vipengele vya mazingira
|
Vitu vyote vya asili na vilivyotengenezwa na binadamu vinaweza kupatikana nyumbani, shuleni, au mahali popote. Binadamu hutegemea mazingira kufanya shughuli zake zote zinazomwezesha kuishi. Hivyo, binadamu ana wajibu wa kutunza na kuhifadhi mazingira kwa matumizi endelevu. Kielelezo namba 3 kinaonesha baadhi ya vitu vinavyopatikana katika mazingira.
Kielelezo namba 3: Baadhi ya vitu vinavyopatikana katika
mazingira
|
Mazingira ya shule yetu
Kazi ya kufanya namba 1
Chunguza vitu vilivyomo katika mazingira ya shule, kisha:
1. Bainisha vitu vya asili na visivyo vya asili ulivyoviona; na
2.
Eleza faida ya vitu ulivyovibaini.
Mazingira ya shule ni vitu vyote vinavyopatikana shuleni. Vitu hivyo
ni kama vile madarasa, ofisi za walimu, nyumba za walimu, miti,
bustani za maua, viwanja vya michezo, bendera ya taifa, na vyoo vya
wanafunzi na vya walimu. Pia, mazingira ya shule yanaweza kuwa na
mabweni, maktaba, maabara za masomo na vitu vinginevyo vya asili kama
vile mito na vilima. Ndani ya darasa kunaweza kuwa na vitu kama vile
madawati, viti, meza, vitabu, ubao na vifaa vingine vya kufundishia na
kujifunzia. Vilevile, wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine wa
shule ni
sehemu ya mazingira ya shule.
Mazingira ya shule moja yanaweza kutofautiana au kufanana na ya shule nyingine kutokana na vitu vilivyomo katika shule husika. Kimsingi, vitu vinavyounda mazingira ya shule vina umuhimu katika ufundishaji na ujifunzaji hivyo, vinapaswa kutunzwa.
Kazi ya kufanya namba 2
Chunguza Kielelezo namba 4, kisha jibu maswali yanayofuata:
Kielelezo namba 4: Mazingira ya shule
|
Maswali
1. Ni vitu gani unaviona katika Kielelezo namba 4?
2. Ni vitu gani muhimu ukiviondoa katika Kielelezo namba 4 vitaathiri
mazingira ya shule? Toa sababu.
Mazingira ya nyumbani
Kazi ya kufanya namba 3
Chunguza Kielelezo namba 5, kisha jibu maswali yanayofuata:
Kielelezo namba 5: Mazingira ya nyumbani
|
Maswali
1. Ni vitu gani unaviona katika Kielelezo namba 5?
2. Ni vitu
gani katika Kielelezo namba 5, vipo katika mazingira ya nyumbani
kwenu?
Mazingira ya nyumbani ni vitu vyote vinavyopatikana mahali tunapoishi. Vitu hivyo vinaweza kuwa nje au ndani ya nyumba. Mazingira ya nje ya nyumba yanaweza kuwa na vitu kama miti, magari, maua, ndege, wadudu, wanyama, mito, milima, mabonde na vitu vingine kulingana na mahali tunapoishi. Pia, mazingira ya ndani ya nyumba yanaweza kuwa na vitu kama kitanda, makochi, vyombo vya kupikia, vifaa vya usafi, pamoja na vitu vingine vyote vinavyopatikana ndani ya nyumba.
Kwa kawaida, mazingira yanaweza kufanana au kutofautiana kutokana na vitu vinavyopatikana katika eneo hilo. Hivyo, siyo lazima mazingira ya nyumba moja yafanane na ya nyumba nyingine. Pia, siyo lazima mazingira ya eneo moja yafanane na ya eneo lingine.
Zoezi la 1
1. Eleza tofauti iliyopo baina ya mazingira ya nyumbani na mazingira ya shuleni.
2. Mazingira ya nyumbani yanaweza kubadilika kutokana na shughuli mbalimbali zinazofanyika nyumbani.
(a) Eleza shughuli zinazoweza kuboresha mazingira ya nyumbani kwenu.
(b) Eleza shughuli zinazoweza kuharibu mazingira ya nyumbani kwenu.
Kazi ya kufanya namba 4
Ukiwa unaelekea shuleni kwako fanya yafuatayo:
1. Chunguza mazingira ya njia unayopita kuelekea shuleni kwako.
2. Bainisha vitu unavyoviona.
3. Bainisha vitu ulivyoviona ambavyo havipo katika mazingira ya nyumbani kwenu.
Uhusiano wa Jiografia na Mazingira
Jiografia na Mazingira ni dhana zinazohusiana na ni vigumu kuzitenganisha. Tumejifunza kwamba mazingira ni vitu vyote vinavyotuzunguka, wakati Jiografia inapambanua kuhusu vitu hivyo. Kwa hiyo, Jiografia inatupatia uelewa kuhusu mazingira yanayomzunguka binadamu na namna tunavyoweza kuhusiana nayo. Vitu kama vile misitu, milima, maziwa, mito, bahari, hali ya hewa, ardhi, na wanyama ni sehemu ya Jiografia na Mazingira. Kwa hiyo, ni muhimu kujifunza dhana hizi mbili kwa pamoja.
Kazi ya kufanya namba 5
Chunguza Kielelezo namba 6, kisha jibu maswali yanayofuata:
Kielelezo namba 6: Shughuli mbalimbali katika
mazingira
|
Maswali
1. Bainisha shughuli zinazofanyika katika Kielelezo namba 6.
2.
Eleza mazingira ambayo shughuli hizo hufanyika.
3. Ni shughuli
zipi ulizozibaini katika Kielelezo namba 6 hufanyika katika mazingira
unayoishi?
4. Kwa nini baadhi ya shughuli katika Kielelezo namba
6, hazifanyiki katika mazingira unayoishi?
Umuhimu wa kujifunza Jiografia na Mazingira
Kujifunza Jiografia na Mazingira kunatuwezesha kuyaelewa mazingira yetu. Pia, Jiografia na mazingira inatuwezesha kutambua rasilimali zilizopo katika mazingira yetu na namna ya uzitumia, kuzitunza na kuzilinda. Mifano ya rasilimali hizo ni wanyama pori, mito, maziwa, bahari, misitu, ardhi, madini na milima. Vilevile, kujifunza Jiografia na Mazingira kunatuwezesha kujua shughuli za binadamu zinazoweza kufanyika katika maeneo mbalimbali. Mfano, maeneo yenye mito, maziwa, na bahari yanaweza kutumika kufanya shughuli za uvuvi, usafiri wa majini au utalii. Maeneo ya tambarare yenye udongo wa rutuba na mvua ya kutosha yanafaa zaidi kwa kilimo na ufugaji. Maeneo yenye misitu yanaweza kutumika kufanya shughuli za kupasua mbao na ufugaji wa nyuki.
Aidha, kujifunza Jiografia na Mazingira kunatuwezesha kuelewa kuhusu hali ya hewa na tabianchi iliyopo mahali fulani. Mfano, eneo lenye miti mingi huwa na hali ya hewa nzuri na mandhari yenye kuvutia. Vilevile, maeneo yenye milima yanaweza kuwa na hali ya hewa yenye baridi kwa sababu ya mwinuko mkubwa. Binadamu hulazimika kuvaa nguo nzito kama sweta kujikinga na baridi. Maeneo ya Tanzania yaliyopo karibu na mwambao wa bahari mara nyingi huwa na hali ya joto zaidi kuliko maeneo ya bara. Hivyo, watu katika maeneo hayo wanaweza kuvaa nguo nyepesi ili kuepuka au kupunguza madhara ya joto. Hata hivyo, hali ya joto katika maeneo ya pwani inaweza kutofautiana kutegemeana na mwinuko wa ardhi na mwelekeo wa upepo.
Jiografia na Mazingira inasaidia kubaini na kuelewa majanga ya asili kama vile mafuriko na vimbunga, na jinsi ya kuepuka athari za majanga hayo. Pia, inasaidia katika kupanga na kutekeleza ujenzi wa miundombinu na huduma za jamii. Mifano ya miundombinu na huduma za jamii ni barabara, hospitali, na shule. Hivyo, elimu ya Jiografia na Mazingira, inamwezesha binadamu kujua maeneo yanayohitaji kupatiwa huduma hizo. Kwa ujumla, kuna umuhimu wa kujifunza somo la Jiografia na Mazingira ili kuwa na matumizi sahihi na endelevu ya vitu vilivyomo katika mazingira. Mfano, matumizi endelevu ya maji, misitu na ardhi.
Zoezi la 2
1. Kwa nini tunajifunza kuhusu Jiografia na Mazingira?
2. Uelewa
kuhusu majanga ya asili unasaidia nini?
3. Ni rasilimali zipi za
asili zinapatikana katika mazingira unayoishi?
Zoezi la marudio
Chagua herufi ya jibu sahihi
1. Mazingira ya asili yanaweza kuwa endelevu kwa kufanya nini?
- Kuchimba madini
- Kuyatunza na kuyahifadhi
- Kujenga nyumba za kisasa
- Kuanzisha viwanda
2. Unaweza kufanya shughuli gani tofauti na uvuvi kama unaishi maeneo yenye mito, mabwawa, na maziwa?
- Kilimo cha umwagiliaji
- Uvunaji wa mazao
- Utengenezaji wa mbao
- Uwindaji na uuzaji wa ngozi
3. Jiografia na Mazingira inasaidia kupata ufahamu wa namna binadamu anavyoweza ______
- kuhusiana na vitu vinavyomzunguka
- kutengeneza mizinga ya nyuki
- kupanga mtawanyiko wa vitu katika mazingira
- kutengeneza samaki
4. Tabianchi ya sehemu moja hutofautiana na ya sehemu nyingine kwa sababu ya_________
- watu waliopo katika mazingira
- sura ya nchi na uoto uliopo katika mazingira
- wanyama waliopo katika mazingira
- wadudu waliopo katika mazingira
5. Ufugaji wa nyuki hutegemea uwepo wa rasilimali gani muhimu?
- Maji, majani na miamba
- Miti, maua na misitu
- Milima, mabonde na bahari
- Mvua, magogo na majani
6. Maeneo ya Tanzania yaliyopo karibu na bahari mara nyingi huwa na hali ya hewa gani?
- Baridi
- Baridi na joto
- Joto
- Unyevunyevu
7. Jirani na nyumbani kwenu kuna mto wenye maji mnayoyatumia katika matumizi mbalimbali. Je, ni ujuzi gani katika Jiografia na Mazingira utakuwezesha kuwa na matumizi endelevu ya mto huo?
- Hali ya hewa
- Utunzaji wa mazingira
- Kilimo cha umwagiliaji
- Uvuvi na utalii
Maswali ya majibu mafupi
8. Tunapata faida gani kwa kupanda miti katika mazingira ya shule?
9. Endapo mzazi au mlezi wako atanunua eneo kubwa lenye msitu, utamshauri afanye shughuli gani?
10. Ni sababu zipi za kijiografia na kimazingira zitakuongoza kuchagua
eneo la kuanzisha kilimo?
11.Jiografia inatuwezesha
kufahamu namna sahihi ya kutumia vitu vilivyopo katika mazingira.
Bainisha matumizi sahihi ya ardhi katika mazingira unayoishi.
Msamiati
- Ardhi sehemu ngumu ya uso wa dunia ambayo haijafunikwa na maji.
- Bahari eneo kubwa la maji ya chumvi ambalo hufunika sehemu kubwa ya uso wa dunia.
- Bustani eneo lililopandwa miti, maua, nyasi, matunda au mbogamboga.
- Hali ya hewa hali ya anga katika eneo fulani maalumu kwa wakati fulani.
- Miundombinu jumla ya njia za usafiri, majengo na huduma ambazo hutoa msingi na usaidizi wa shughuli mbalimbali katika eneo maalumu.
- Rasilimali vitu muhimu na vya thamani vilivyopo katika mazingira.
- Shughuli za binadamu kazi au matendo mbalimbali ambayo watu hufanya katika maisha yao ya kila siku.
Sura ya 02 :Sura ya nchi
Utangulizi Uso wa dunia umefunikwa kwa tabaka gumu ambalo huitwa ardhi. Ardhi ina maumbo mbalimbali. Maumbo hayo huunda sura ya nchi ya eneo fulani. Katika sura hii utajifunza kuhusu maana ya sura ya nchi, maumbo makuu ya sura ya nchi, mtawanyiko na umuhimu wa maumbo ya sura ya nchi. Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kuhusiana vema na maumbo ya sura ya nchi yaliyopo katika mazingira unayoishi. |
Fikiri
Maumbo tofauti ya ardhi uliyowahi kuyaona
Maana ya sura ya nchi
Sura ya nchi ni mwonekano wa maumbo mbalimbali ya ardhi katika uso wa dunia. Maumbo haya huunda mandhari tofauti za sehemu mbalimbali. Sura ya nchi huwa na mtawanyiko wa maumbo kama vile milima, vilima, tambarare, uwanda wa juu, besini na mabonde. Shughuli za binadamu kama vile kilimo, ujenzi wa makazi, na ufugaji hutegemea maumbo ya sura ya nchi ya mahali fulani. Hivyo, ni muhimu kuyafahamu maumbo ya sura ya nchi ili tuweze kuhusiana nayo kwa njia ambayo ni endelevu.
Kazi ya kufanya namba 1
1. Chunguza Kielelezo namba 1, kisha bainisha maumbo ya sura ya nchi yaliyopo katika kielelezo hicho.
Kielelezo namba 1: Maumbo mbalimbali ya sura ya
nchi
|
2. Chunguza na eleza maumbo ya sura ya nchi yaliyopo katika mazingira unayoishi.
Maumbo makuu ya sura ya nchi
Kazi ya kufanya namba 2
Tumia vyanzo vya mtandaoni kutafuta video zinazohusu maumbo makuu ya sura ya nchi ya Tanzania. Angalia au sikiliza video hizo kisha, andika ufupisho.
Sura ya nchi ya mahali hutokana na uwepo wa maumbo mbalimbali ya ardhi katika eneo husika. Maumbo hayo hujulikana kama maumbo ya sura ya nchi. Maumbo ya sura ya nchi hutofautiana kimuonekano kulingana na urefu na umbo. Ili kuelewa tofauti za maumbo ya ardhi katika maeneo mbalimbali, inatupasa kujifunza kuhusu maumbo makuu ya sura ya nchi. Maumbo hayo ni milima, mabonde, vilima, uwanda wa juu, besini na tambarare. Kielelezo namba 2 kinaonesha muonekano wa maumbo makuu ya sura ya nchi.
Kielelezo namba 2: Maumbo makuu ya sura ya nchi
|
Mtawanyiko na umuhimu wa maumbo makuu ya sura ya nchi ya Tanzania Kila eneo la ardhi lina sura yake kutokana na maumbo mbalimbali yanayoonekana. Kwa mfano, sura ya nchi ya Tanzania ni ya kipekee kutokana na muonekano wake. Uwepo wa milima, mabonde, tambarare, vilima, besini, na uwanda wa juu ni fahari ya Tanzania. Maumbo haya yote hupatikana katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Kazi ya kufanya namba 3
Tumia vitabu na vyanzo vya mtandaoni, soma au sikiliza kuhusu mtawanyiko wa maumbo makuu ya sura ya nchi ya Tanzania. Kisha, bainisha shughuli zinazofanyika katika maumbo ya sura ya nchi ya Tanzania na yale yaliyopo katika mazingira unayoishi.
Mlima
Mlima ni umbo la ardhi lenye mwinuko mrefu zaidi juu ya uso wa dunia. Sehemu ya juu ya mlima huitwa kilele cha mlima. Kilele cha mlima kinaweza kuwa na theluji au barafu au kisiwe nazo. Pia, mlima huwa na miteremko mikali. Tanzania ina milima mingi inayotofautiana kwa urefu. Mfano; mlima mrefu kuliko yote Tanzania ni mlima Kilimanjaro, ambao upo katika mkoa wa Kilimanjaro. Mlima Kilimanjaro una urefu wa mita 5,895. Kilele cha mlima Kilimanjaro kimefunikwa na barafu na theluji. Hii ni kwa sababu kadiri mwinuko wa ardhi unavyoongezeka joto hupungua. Pia, mlima Kilimanjaro ni wa kwanza kwa urefu barani Afrika. Kielelezo namba 3 kinaonesha mandhari ya mlima Kilimanjaro.
Kielelezo namba 3: Mlima Kilimanjaro
|
Milima mingine iliyopo Tanzania ni mlima Meru uliopo mkoa wa
Arusha wenye urefu wa mita 4,566, na mlima Rungwe uliopo mkoa wa
Mbeya wenye urefu wa mita 2,981. Milima mingine ni safu za
milima ya Uluguru iliyopo mkoa wa Morogoro yenye urefu wa mita
2,630, na safu za milima ya Usambara iliyopo mkoa wa Tanga
yenye
urefu wa mita 2,290.
Vilima
Vilima ni umbo la ardhi lililoinuka kwa urefu wa wastani. Vilima vina urefu mdogo kuliko milima na havina miteremko mikali kama milima. Hata hivyo vilima vina kilele kama mlima. Vilima hupatikana katika maeneo mbalimbali ya Tanzania. Mfano wa vilima ni kama vile: vilima vya Ngorongoro vilivyoko Arusha, vilima vya Mererani vilivyoko Manyara, vilima vya Sao na Kitonga vilivyoko Iringa. Pia, kuna vilima vya Sekenke vilivyoko mkoa wa Singida. Kielelezo namba 4 kinaonesha vilima.
Kielelezo namba 4: Vilima
|
Umuhimu wa milima na vilima
Maumbo mbalimbali ya sura ya nchi ni muhimu katika maisha ya binadamu. Mara nyingi, milima, na vilima huwa ni vyanzo vizuri vya maji. Maji hayo hutumiwa na binadamu na viumbe wengine kwa matumizi mbalimbali. Pia, milima husababisha aina mojawapo ya mvua. Vilevile, milima na vilima ni sehemu za vivutio vya utalii. Watalii hupanda milimani na vilimani kuona misitu, maporomoko ya maji na viumbe mbalimbali wa porini. Aidha, watu hujipatia kipato kutokana na shughuli za utalii. Kielelezo namba 5 kinaonesha maporomoko ya maji kutoka kwenye vilima.
![]() Kielelezo namba 5: Maporomoko ya maji |
Pia, katika miteremko ya milima, kuna misitu minene yenye wanyama ambao ni vivutio vya utalii. Vilevile, miti iliyopo katika misitu hiyo inatupatia mbao, na vifaa vingine vya ujenzi. Baadhi ya miti ni dawa zinazotumiwa na binadamu kutibu magonjwa mbalimbali.
Zoezi la 1
Chagua herufi ya jibu sahihi
1. Zipi kati ya sifa zifuatazo zinatofautisha mlima na
kilima?
(a) Urefu na miteremko
(b) Urefu na rutuba
(c)
Miamba na udongo
(d) Ufupi na wingi wa theluji
2. Kwa nini vilele vya baadhi ya milima kama vile mlima Kilimanjaro vimefunikwa na barafu?
(a) Kuna joto kali
(b) Kuna mvua nyingi
(c) Kuna
baridi kali
(d) Kuna maji mengi
Maswali ya majibu mafupi
3. Unafikiri ni changamoto zipi wanazozipata mafundi wa ujenzi wanapojenga nyumba maeneo yenye vilima au milima?
4. Athari zipi za mazingira zitatokea endapo kilimo kitafanyika kwenye miteremko ya milima?
5. Ni milima gani ipo katika mikoa ifuatayo:
(a) Arusha
(b) Mbeya
(c) Morogoro
Mabonde
Mabonde ni maumbo ya ardhi yenye kina kirefu. Mara nyingi mabonde huwa katikati ya milima au vilima kama inavyooekana katika Kielelezo namba 6.
Kielelezo namba 6: Bonde
|
Baadhi ya mabonde huwa na maji ambayo hutengeneza mito, mabwawa au maziwa. Mfano, katika nchi ya Tanzania kuna bonde kuu la ufa la Afrika Mashariki. Katika bonde hilo, kuna Ziwa Natron lililopo mkoa wa Arusha, Ziwa Eyasi na Manyara yaliyopo mkoa wa Manyara. Pia, kuna Ziwa Tanganyika linalopatikana katika mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa. Ziwa Tanganyika lina kina kirefu kuliko maziwa yote yanayopatikana Tanzania na Afrika kwa ujumla. Vilevile kuna Ziwa Nyasa linalopatikana mikoa ya Ruvuma, Njombe na Mbeya.
Umuhimu wa mabonde
Mabonde ni muhimu kwa sababu hukusanya maji kutoka kwenye milima na vilima. Hii inayafanya mabonde kuwa vyanzo vya maji. Sehemu zenye mabonde zilizo na maziwa, mito na mabwawa ni makazi ya viumbe wa majini wakiwemo samaki. Hivyo, sehemu hizi hutumika kwa shughuli za uvuvi. Pia, maeneo yenye mabonde ya mito huwa na udongo wenye rutuba hivyo hutumika katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji. Vilevile, mito na mabwawa hutumika kuzalisha umeme. Aidha, maziwa na baadhi ya mito hutumika kwa usafiri wa vyombo vya majini kama vile meli na boti.
Uwanda wa Juu
Uwanda wa juu ni sehemu ya ardhi yenye mwinuko wenye umbo la tambarare. Kielelezo namba 7 kinaonesha uwanda wa juu.
Kielelezo namba 7: Uwanda wa juu
|
Nyanda za juu zinaweza kutofautiana kwa umbo na kwa ukubwa. Mfano wa uwanda wa juu Tanzania ni uwanda wa juu wa kusini ambao unapatikana katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe, na Njombe.
Umuhimu wa uwanda wa juu
Baadhi ya maeneo ya uwanda wa juu hutumika kujenga makazi na kuhifadhiwa kama vivutio vya utalii kutokana na uzuri wa mandhari na hali ya hewa. Mfano, hifadhi ya taifa ya Kitulo ipo katika uwanda wa juu kusini mwa Tanzania katika mikoa ya Mbeya na Njombe. Hifadhi hii ipo kati ya vilele vya milima ya Kipengele, Uporoto na Safu za milima ya Livingstone. Hii ni hifadhi ya kwanza barani Afrika kuanzishwa kwa lengo la kutunza mimea yake ya asili jamii ya maua. Sehemu nyingine ya uwanda wa juu hutumika kwa kilimo.
Tambarare
Tambarare ni umbo la ardhi lisilokuwa na miinuko. Maeneo tambarare hayana milima, vilima, au miinuko mikubwa. Sehemu kubwa ya tambarare huwa na ardhi inayofanana kwa mwinuko wake kwa kiasi kikubwa kama inavyoonekana katika Kielelezo namba 8. Mifano ya maeneo tambarare Tanzania ni baadhi ya maeneo ya mbuga ya Serengeti na Tarangire.
Kielelezo namba 8: Tambarare
|
Umuhimu wa maeneo ya tambarare
Sehemu za tambarare huwa na udongo wenye rutuba unaofaa kwa kilimo na shughuli za ufugaji. Kielelezo namba 9 kinaonesha kilimo katika eneo tambarare.
Kielelezo namba 9: Kilimo katika eneo tambarare
|
Pia, sehemu za tambarare hutumika kujenga makazi ya watu, na miundombinu mingine kwa kuwa maeneo haya hayahitaji usawazishaji mkubwa wa ardhi kwa vile hayana vilima na miinuko. Vilevile, maeneo ya tambarare ni mazuri kwa shughuli za michezo na usafiri wa ardhini. Aidha, maeneo haya yanaweza kuwa na misitu inayohifadhi wanyama na viumbe wengine wa porini ambao pia ni vivutio vya utalii.
Besini
Hii ni sehemu ya ardhi iliyobonyea na kutengeneza umbo kama la beseni. Besini inaweza kuwa na maji au kutokuwa na maji. Besini yenye maji hutengeneza ziwa. Mfano wa besini yenye maji ni Ziwa Viktoria lililopo mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Simiyu, na Geita. Ziwa Viktoria ni kubwa kuliko maziwa yote yanayopatikana Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Zoezi la 2
1. Eleza tofauti zilizopo kati ya Ziwa Viktoria na
Tanganyika.
2. Ni mikoa ipi ya Tanzania iliyopo katika
uwanda wa juu kusini?
3. Ni katika umbo lipi la sura ya
nchi utapendelea zaidi kujenga nyumba yako? Kwa nini?
4.
Unafikiri nini kitatokea endapo watu watajenga nyumba jirani na
maeneo yenye mabonde?
Zoezi la marudio
Chagua herufi ya jibu sahihi
1. Ni katika umbo gani la sura ya nchi kati ya yafuatayo linaweza kusababisha kutokea kwa aina mojawapo ya mvua?
(a) Tambarare
(b) Bonde
(c) Mlima
(d) Besini
2. Safu za milima ya Usambara zinapatikana katika mkoa gani?
(a) Kilimanjaro
(b) Morogoro
(c) Tanga
(d) Mbeya
3. Oanisha safu A na safu B ili kuleta maana.
Safu A | Safu B |
i. Mlima | A. ardhi iliyoinuka kwa urefu wa wastani na haina miteremko mikali |
ii. Mabonde | B. hakuna milima, vilima, wala miinuko mikubwa |
iii. Tambarare | C. una kimo kirefu zaidi kilichoinuka juu ya uso wa dunia |
iv. Vilima | D. hutokea katikati ya milima au vilima |
Maswali ya majibu mafupi
4. Ni vitu gani vinavyotofautisha sura ya nchi ya mahali?
5. Bainisha kwa mifano maumbo makuu ya sura ya nchi yanayopatikana katika mikoa ifuatayo:
(a) Iringa
(b) Morogoro
(c) Mwanza
(d) Kigoma
(e)
Kilimanjaro
(f) Singida
6. Tumia mifano halisi kueleza umuhimu wa maumbo ya sura ya nchi ya Tanzania.
Msamiati
- Makazi sehemu ambapo watu huishi na kujenga nyumba zao
- Mwinuko sehemu ya ardhi iliyoinuka kuliko maeneo mengine
- Uso wa dunia sehemu ya nje ya dunia inayojumuisha maeneo ya nchi kavu na maji
- Utalii Matembezi yanayohusisha watu kwenda kutembelea maeneo nje ya mazingira yao ya kawaida kwa lengo la kupumzika, biashara au kujifunza
- Ziwa sehemu kubwa ya maji ambayo kwa kawaida huzungukwa na nchi kavu